"LET THERE BE LIGHT" Ministries
home  |  Tanzanian Tracts

HEKALU  LA  MUNGU  LINAHITAJI  KUTAKASWA!?

     Patakatifu pekee pa Mungu palipopata kuwepo duniani, ambapo Biblia hutoa habari zake, palikuwa ni sehemu ile ambayo Mungu alimwamuru Musa kujenga: “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kuwa kati yao” (angalia Kutoka 25:8). Hapa palitajwa na Paulo kuwa Patakatifu pa agano la kwanza (angalia Waebrania 9:1). Lakini je, agano jipya halina Patakatifu? “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu wa mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu.” Waebrania 8:1-2.
     Hapa patakatifu pa agano jipya panafunuliwa--hema ya mbinguni. Patakatifu pa duniani pa agano la kwanza pilifanywa na mwanadamu na kujengwa na Musa. Lakini hapa patakatifu pa mbinguni pamewekwa na Bwana na siyo mwanadamu. Katika Patakatifu pa agano la kwanza makuhani wa kidunia waliendesha huduma [utumishi]. Katika Patakatifu pa mbinguni pa agano jipya, Kristo, Kuhani wetu Mkuu, anahudumu mkono wa kuume wa Mungu. Hivyo, Patakatifu petu palikuwa duniani, pengine pako mbinguni.
     Patakatifu palipojengwa na Musa palifanywa kufuatisha kielelezo cha hekalu la mbinguni. Bwana alimwelekeza Musa: “Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya….Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.” Kutoka 25:9, 40 (angalia pia Waebrania 9:23, 8:5). Hii ilifanyika kusudi imani yetu iweze kushika ukweli kwamba mbinguni kuna Patakatifu ambapo huduma zake zinafanywa kwa ajili ya ukombozi wa jamii ya mwanadamu. Patakatifu hapa ambamo Kristo anahudumu kwa niaba yetu, ndipo chanzo kikuu, ambacho hekalu lililojengwa na Musa lilikuwa ni nakala tu.
     Ibada zote katika Patakatifu pa duniani zilikuwa ni kwa ajili ya kufundisha ukweli kuhusiana na Patakatifu pa mbinguni. Wakati maskani ya duniani ilipokuwa inasimama, njia kuingia katika maskani ya mbinguni ilikuwa bado haijadhihirishwa (angalia Waebrania 9:8). Lakini wakati Kristo aliposulubiwa, pazia la Patakatifu pa duniani lilipasuka vipande viwili likiashiria kwamba njia mpya na nzuri zaidi ilikuwa inawekwa (angalia Mathayo 27:51; Luka 23:45). Njia ya kwanza ilikuwa inaondolewa kusudi ya pili, iliyojengwa katika msingi wa ahadi nzuri zaidi, ingeweza kuanzishwa (angalia Waebrania 8:6). Wakati Kristo alipokuwa duniani, asingekuwa kuhani (angalia Waebrania 8:4), na hivyo asingeweza kutoa damu yake iliyomwagika na kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. Lakini Kristo alifufuka kutoka kwa wafu, akapaa mbinguni, na kisha akawa Kuhani wetu Mkuu ili kusudi aweze kupeleka mbele za Baba damu yake mwenyewe iliyomwagika kwa ajili yetu, na katika hali hiyo kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi. Kwa hiyo upatanisho usingekuwa umekamilishwa au kumalizika msalabani, lakini ungeanza tu baada ya Kristo kupaa mbinguni na kuanza kazi yake ya huduma katika Patakatifu pa mbinguni kama Kuhani wetu Mkuu.
     Mungu alifunua badiliko hili kuu kuanzia Patakatifu pa duniani kwenda katika Patakatifu pa mbinguni kupitia manabii wake--na hasa kupitia mtume wake mpendwa Yohana (Ufunuo 4:1-5, 8:3-4, 9:13, 11:19, 14:17-18, 15:5-8).
     Siyo tu kwamba Kristo anasihi kwa ajili ya damu yake ya thamani mbele za Baba katika patakatifu pa mbinguni kwa ajili yako na mimi (angalia Waebrania 9:11-14, 24-28), lakini pia kinaonekana kiti cha enzi kikuu cha Mungu, ambacho kimezungukwa na majeshi ya mbinguni, wote wakingoja kutii amri za Mungu (angalia Zaburi 103:19-20). Kutoka katika hekalu hili la Mungu malaika hawa wanatumwa kujibu maombi ya watoto wake hapa duniani (angalia Danieli 9:21-23; Waebrania 1:7, 14).
     Hivyo, Patakatifu pa mbinguni panaonekana kuwa kituo kikuu cha mambo ambapo kutoka hapo nguvu zote za Mungu muhimu kwa ajili ya kushinda kila jaribu la Shetani hutumwa kwa kila mmoja ambaye ameshikamana pamoja nayo kwa imani. Kristo, Kuhani wetu Mkuu aliye juu ambaye anahudumu kwa ajili yetu anatamani kunyosha mkono wake kutoka katika Patakatifu hapa na pa mbinguni ili kwa upendo apate kumshika kila ambaye anafika juu kwa njia ya imani na kuchukua msaada unaotolewa kwao. Mtu yule ambaye imani yake inachukua Msaada Mkuu, anaweza kupita kwa usalama katika kilima kikali cha dhiki, nafsi yake mwenyewe ikiwa imejazwa na nuru wakati ikitoa nuru na baraka kwa wengine. Kadiri ambavyo yeye, kwa imani, anamshikilia kwa nguvu Mungu, anayo nuru na nguvu kutoka Patakatifu pa mbinguni juu: lakini kama akiruhusu mashaka na kutoamini kuvunja mshikamano huu, yuko gizani, siyo tu kutoweza kusonga mbele peke yake, lakini kuzuia njia ya wengine hali kadhalika.
     Kutakuja kuwepo na wakati ambao kazi ya huduma ya Kristo itakoma na hatatoa tena damu yake kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu (angalia Danieli 12:1; Ufunuo 22:11-12). Hii itaanzisha wakati wa taabu ambao utazijaribu nafsi za wanadamu, na kama tungechagua kufanya dhambi baada ya kipindi hiki, haitakuwepo njia ambapo dhambi inaweza kusamehewa na tutakuwa tumepotea! Kwa sababu jambo hili ni la wokovu--uzima au mauti, kuna njia yoyote tunapoweza kujua kipindi ambapo kazi ya huduma ya Kristo itakoma ili kusudi tuweze kujiweka tayari wenyewe kwa wakati huu? Ndiyo! Kabla ya kazi ya maombezi ya Kristo kufikia mwisho, patakatifu pa mbinguni lazima patakaswe.
     Kutakaswa kwa Patakatifu, pote pawili katika huduma ya duniani na mbinguni, lazima pakamilishwe kwa damu: pa kwanza, kwa damu ya wanyama; pa baadaye, kwa damu ya thamani ya Kristo. Hii ilikuwa ni muhimu kwa sababu bila kumwaga damu, lisingekuwepo ondoleo la dhambi (angalia Waebrania 9:22). Ondoleo, au kuweka mbali dhambi, ni kazi ya mwisho kukamilishwa. Lakini ni namna gani dhambi ingekuwa imeshikamanishwa pamoja na Patakatifu, iwe mbinguni au duniani? Hili laweza kujifunzwa kwa kuchunguza huduma ya mfano ya patakatifu pa duniani; kwani makuhani ambao walihudumu duniani, walihudumu kwa “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni.” Waebrania 8:5.
     Kuhudumu katika Patakatifu pa duniani kulikuwa na sehemu mbili; makuhani walihudumu kila siku katika sehemu takatifu [chumba kitakatifu], wakati ambapo siku moja tu kwa mwaka kuhani mkuu alifanya kazi maalum ya upatanisho katika sehemu takatifu mno [Patakatifu pa Patalatifu] kwa ajili ya kutakasa Patakatifu (angalia Law 16). Siku kwa siku mdhambi aliyetubu alileta matoleo yake kwenye mlango wa hema ya kukutania, na akiweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama, alitubia dhambi zake, hivyo kwa mfano akizihamisha kutoka kwake mwenyewe kwa kafara asiye na hatia. Kisha mnyama alichinjwa, akimwaga damu yake na hivyo, katika mfano, kuleta ondoleo la dhambi. Sheria iliyovunjwa ya Mungu ilihitaji uhai wa mwenye dhambi. Damu, ikiwakilisha uzima wa mdhambi uliotolewa, ambaye hatia yake mnyama aliibeba, ilichukuliwa na kuhani kwenye sehemu takatifu na kunyunyiziwa mbele ya pazia la Patakatifu pa Patakatifu ambapo lilikuwapo sanduku [la agano] lililokuwa na sheria ya Mungu ambayo mdhambi alikuwa ameiasi. Kwa utaratibu kama huu dhambi ilikuwa, kupitia damu, imehamishwa kwa mfano kwenda Patakatifu.
     Hiyo ndiyo iliyokuwa kazi iliyoendelea, siku kwa siku, kwa mwaka mzima. Dhambi za watu wa Mungu zilikuwa kwa namna hiyo zimehamishiwa katika Patakatifu, na kazi maalum ililazimu ili ziondolewe. Mungu aliamuru kwamba upatanisho ufanyike kwa kila chumba cha sehemu hizi mbili takatifu za Patakatifu. “Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja na katikati ya machafu yao.” Upatanisho pia ulitakiwa kufanywa kwa ajili ya madhabahu, na “kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.” Law 16:16, 18-19.
     Mara moja kila mwaka, katika Siku kuu ya Upatanisho, kuhani mkuu aliingia Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kutakasa hema takatifu. Kazi iliyofanyika pale ilimaliza mizunguko ya kila mwaka ya kuhudumu. Katika Siku ya Upatanisho mbuzi wawili waliletwa kwenye mlango wa hema ya kukutania--mmoja kwa ajili ya Bwana, na wa pili kwa ajili ya Azazeli (angalia Law 16:8). Mbuzi aliyechaguliwa kwa ajili ya Bwana alitakiwa kuchinjwa kama sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu. Na kuhani alitakiwa kuleta damu yake ndani ya pazia katika Patakatifu pa Patakatifu na kuinyunyiza mbele na juu ya kiti cha rehema. Damu pia ilitakiwa kunyunyiziwa juu ya madhabahu ya uvumba katika chumba cha kwanza.
     Juu ya kichwa cha Azazeli kuhani mkuu alitubia dhambi zote zilizosamehewa na uovu wa watu wa Mungu ambao ulikuwa umejazana mpaka wakati huo, hivyo akiuweka au kuuhamishia juu ya Azazeli. Kisha mbuzi huyu aliongozwa mbali kwa mkono wa mtu aliye tayari kwenda jangwani, na hakurudi tena (angalia Law 16:21-22). Patakatifu hatimaye palikuwa pametakaswa na kuwekwa huru kutoka katika dhambi. Hakukuwepo na muda uliowekwa kwa ajili ya kazi ya upatanisho kumalizika katika siku hiyo, lakini muda uliochukuliwa uliamuriwa kutokana na jinsi tukio lilivyomchukua kuhani mkuu kumaliza kazi yake (angalia Law 16:17). Lingeweza kukamilika muda wowote katika siku hiyo.
     Utaratibu huu wote ulikuwa umepangwa kuwahamasisha watu wa Mungu kwa utakatifu wa Mungu na namna anavyochukia dhambi; na, zaidi, kuwaonyesha wao kuwa wasingeshikamana na dhambi pasipo kuchafuliwa. Kila mmoja alitakiwa kutesa nafsi yake wakati kazi hii ya upatanisho ilipokuwa inaendelea. Kusanyiko zima lilitakiwa kutumia siku nzima katika kujidhiri kikamilifu mbele za Mungu, kwa maombi, kufunga, na kuchunguza kwa kina mioyo.
     Ukweli mkuu na muhimu kuhusiana na upatanisho kwa ajili ya dhambi unafundishwa na hii huduma ya mfano. Mbadala ilikubaliwa katika sehemu ya mdhambi; lakini dhambi haikuondolewa kwa damu ya mnyama. Njia kwa hali hiyo ilitolewa ili kupitia kwa hiyo dhambi ihamishiwe Patakatifu. Kwa kutoa damu mdhambi alikiri mamlaka ya sheria, akatubia hatia kwa kuasi sheria, na kueleza tamanio lake kutaka msamaha kwa njia ya imani kwa Mkombozi atakayekuja; lakini alikuwa bado hajawekwa huru kabisa kutoka kwenye hukumu ya sheria. Siku ya Upatanisho kuhani mkuu, akiwa ameshachukua matoleo kutoka kwenye kusanyiko, aliingia katika patakatifu pa patakatifu akiwa na damu ya matoleo haya, na kuinyunyizia juu ya kiti cha rehema, moja kwa moja juu ya sheria, kufanya maridhio ya madai yake. Hatimaye, katika tabia yake ya mpatanishi, alichukua dhambi juu yake mwenyewe akiziondoa kutika Patakatifu. Akiweka mikono yake juu ya kichwa cha Azazeli, hatimaye alitubia juu yake dhambi zote hizi, hivyo kwa mfano akizihamisha kutoka kwake kwenda kwa mbuzi [wa Azazeli]. Kisha mbuzi alizibeba kwenda mbali, na zilihesabiwa kuwa zimetengwa milele kutoka kwa watu.
     Hivyo ndivyo ilivyokuwa huduma iliyofanywa “kwa mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni.” Na kile kilichofanywa katika mfano katika kuhudumu kwenye Patakatifu pa duniani kinafanywa katika hali halisi katika kuhudumu kwenye Patakatifu pa mbinguni leo. Baada ya kupaa kwake Mwokozi wetu alianza kazi yake kama Kuhani wetu Mkuu. Paulo anasema:
     “Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu.” Waebrania 9:24.

     Kuhudumu kwa kuhani mwaka mzima katika chumba cha kwanza cha Patakatifu, au “kile kilicho ndani ya pazia” ambacho kilifanyiza mlango na kutenga sehemu takatifu kutoka kwenye sehemu ya nje, huwakilisha kazi ya kuhudumu ambayo Kristo alianza kuifanya baada ya kusulubiwa kwake na kupaa mbinguni. Ilikuwa ni kazi ya kuhani katika kuhudumu kila siku kuleta mbele za Bwana damu ya matoleo ya dhambi, pia harufu ambayo ilipanda juu pamoja na sala za Israeli. Hivyo ndivyo Kristo alivyosihi kwa damu yake mbele za Baba kwa niaba ya wadhambi, na kuleta mbele yake pia, pamoja na harufu ya thamani ya haki yake mwenyewe, sala za waamini waliotubu. Hiyo ndiyo iliyokuwa kazi ya kuhudumu katika chumba cha kwanza katika Patakatifu mbinguni.
     Hapo ndipo imani ya mitume wa Kristo ilipomfuata kadiri alivyopaa kutoka katika macho yao (angalia Mdo 1:9-11). Hapa ndipo matumaini yao yalipotulia, “matumaini tuliyo nayo,” Paulo alisema, “kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele...Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele.” Waebrania 6:19-20, 9:12.
     Kwa miaka elfu moja na mia nane baada ya kupaa kwa Krsto kazi hii ya kuhudumu iliendelea katika chumba cha kwanza cha Patakatifu pa mbinguni. Damu ya Kristo, ilisihi kwa niaba ya waamini waliotubu, kupata msamaha wao na ukubali kwa Baba, na bado dhambi zao zilibaki kwenye vitabu vya kumbukumbu. Kama katika huduma ya kivuli kulikuwa na kazi ya upatanisho wakati wa kufunga mwaka, kwa hiyo kabla kazi ya Kristo kwa ajili ya ukombozi wa jamii ya mwanadamu kukamilika kuna kazi ya upatanisho kwa ajili ya kuondoa dhambi kutoka kwenye Patakatifu pa mbinguni.
     Kama ilivyokuwa zamani, dhambi za watu kwa imani ziliwekwa juu ya kafara ya dhambi na kupitia katika damu iliyopelekwa, katika mfano, kwenye patakatifu pa duniani, kwa hiyo katika agano jipya dhambi za aliyetubu kwa imani zinawekwa juu ya Kristo na kupelekwa, kwa kweli, kwenye Patakatifu pa mbinguni. Na kama ilivyokuwa katika kivuli cha kukamilisha utakaso wa [Patakatifu] pa duniani kwa kuondolewa kwa dhambi ambazo zilikuwa zimepachafua, kwa hiyo kutakaswa halisi kwa [Patakatifu pa] mbinguni kunatakiwa kukamilishwa kwa kuondolewa, au kufuta kabisa, dhambi ambazo zimewekwa katika kumbukumbu kwenye vitabu vya mbinguni (angalia Zaburi 69:28; Malaki 3:16; Danieli 12:1; Wafilipi 4:3; Ufunuo 3:5, 13:8, 17:8, 22:19). Lakini kabla hili halijaweza kukamilishwa, lazima kuwepo na uchunguzi wa vitabu hivi vya kumbukumbu kuamua ni nani, kwa njia ya toba ya dhambi na imani katika Kristo, wanastahili kufaidi kutokana na upatanisho wake. Kutakaswa kwa Patakatifu kwa hiyo huhusisha kazi ya uchunguzi--kazi ya hukumu (angalia Danieli 7:10; Ufunuo 20:4, 11-15; Mhubiri 12:13-14). Kazi hii inapaswa kufanyika kabla ya kuja kwa Kristo kuwakomboa watu wake; kwani wakati ajapo, ujira wao tayari umeamriwa na upo pamoja na Kristo kumpatia kila mmoja sawasawa na matendo yake (angalia Mathayo 16:27; Ufunuo 22:12). Lakini huduma hii ya mwisho katika chumba cha pili ingetokea lini, Patakatifu kuanza kutakaswa, ambapo baada ya hapo huduma ya Kristo ingeisha?
     “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” Danieli 8:14.

     Katika unabii wa Biblia, kila siku ya muda wa unabii ingekuwa sawa na mwaka mmoja halisi wa wakati (angalia Hesabu 14:34; Ezekieli 4:6). Kwa hiyo siku 2300 za wakati wa unabii zingekuwa sawa na miaka 2300 halisi ya wakati. Lakini ni lini unabii huu ungeanza kusudi tuanze kupiga picha ya tarehe ya mwisho na kuamua ni lini Patakatifu pangeanza kutakaswa? Tunaambiwa katika unabii mwingine ambao unaelekeza kwa Kristo akiwa Masihi, na vile vile Kuhani Mkuu:
     “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu…[na] kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili...Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu...Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hilo ataikomesha sadaka ya dhabihu...” Danieli 9:24-27.

     Historia inafunua kuwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerualemu ilitokea mwaka 457 KK, na hivyo tarehe hii ndiyo mwanzo kwa vyote viwili--majuma 70 (au siku za unabii 490 au miaka halisi) na hali kadhalika unabii wa siku/miaka 2300. Kwa hiyo 457 KK jumlisha majuma 7 (siku/miaka 49) ilituleta moja kwa moja katika historia wakati ambapo hekalu la Yerusalemu lilipojengwa upya mwaka 408 KK. Majuma 62 zaidi (siku/miaka 434) ilituleta moja kwa moja katika historia katika kipindi ambapo Kristo alitiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu kama Masihi mwaka 27 BK (angalia Mathayo 3:13-17; Luka 4:17-21). Juma moja la mwisho lilibaki, na katikati ya kipindi hiki cha mwisho cha miaka 7, au miaka 3½ baada ya Masihi kutiwa mafuta, Kristo alisulubishwa kwa sababu ya dhambi zetu mwaka 31 BK. Haikuwezekana mpaka baada ya miaka iliyobaki 3½ ndipo kifo cha mashahidi wa kwanza wa Wakristo kilipotokea kwa Stefano kupondwa mawe na injili ya ufalme kuhubiriwa kwa Mataifa mwaka 34 BK (angalia Mdo 7, 8:1-8, 18:6). Hili hatimaye lilikatiza majuma 70 siku/miaka 490 ya unabii ambao ulimwonyesha wazi wazi Kristo kuwa ni Masihi na hivyo Kuhani Mkuu aliye juu wa kweli wa watu Mungu, lakini siku/miaka 2300 ya unabii ilikuwa haijakamilika bado. Toa miaka 490 kutoka katika miaka 2300 na tutabakiwa na miaka 1810. Kwa hiyo kugundua ni lini unabii wa siku/miaka 2300 ungeishia na kuhudumu kwa Kristo ambapo angeanza kutakasa Patakatifu pa mbinguni kutoka katika dhambi, tungeweza kuongeza miaka 1810 kwa ile 34 BK ambayo ingetuleta sisi kwenye mwaka 1844.
     Mwishoni mwa unabii wa siku/miaka 2300 katika mwaka wa 1844, Kristo alikoma katika kazi yake ya kuhudumu kwenye chumba cha kwanza na kuingia katika chumba cha Patakatifu mno kufanya kazi ya kufunga upatanisho iliyo muhimu kutakasa Patakatifu kutoka katika dhambi na kukaribisha ujio wake wa pili. Mwaka 1844 Kristo alifunga mlango (au pazia la maingilio) wa chumba cha kwanza na kufungua mlango (au pazia la maingilio) katika chumba cha pili cha Patakatifu pa mbinguni kuanza kazi ya upatanisho (angalia Ufunuo 3:7, 11:19). Kwa miaka mingi sasa, Kristo amekuwa anahudumu katika chumba cha pili akifanya upatanisho kwa dhambi zilizotubiwa na kuachwa za watu wake--kwanza kwa walio kufa (angalia Ufunuo 11:18), na kisha kwa walio hai (angalia Ezekieli 9:1-6; Ufunuo 22:11). Na wakati kazi yake ya Kuhani Mkuu itakapokwisha, ambayo inaweza kuwa wakati wowote sawa na ambavyo haukuwepo wakati uliowekwa, basi Kristo atakoma kufanya upatanisho milele, kisha ataweka dhambi hizi zote juu ya kichwa cha mbuzi wa Azazeli, na wowote wale ambao wanachagua kufanya dhambi baada ya kipindi hiki lazima wao wenyewe wabebe adhabu kamili kwa dhambi yao--ambayo ni mauti ya milele! (angalia Warumi 6:23).
     Wakati matoleo ya dhambi yalielekeza kwa Kristo kama Kafara yetu kuu, na kuhani mkuu alimwakilisha Kristo kama Mpatanishi wetu, mbuzi wa Azazeli angemwakilisha Shetani, mwanzilishi wa dhambi zote, ambaye juu yake dhambi zote za waliotubu kwa moyo wote hatimaye zitawekwa huu yake--hivyo kuziondoa kutoka Patakatifu. Wakati Kristo, kwa wema wa damu yake, huondoa dhambi za watu wake kutoka katika Patakatifu pa mbinguni kwenda kwake mwenyewe pale kwenye kufunga kwa huduma yake, hatimaye ataziweka dhambi hizi juu ya Shetani, ambaye, katika kupitishwa kwa hukumu, lazima achukue adhabu ya mwisho kwa ajili ya dhambi zote. Kama tu mbuzi wa Azazeli alivyopelekwa mbali katika nchi isiyokaliwa na watu, ili asirudi tena katika kusanyiko la Israeli, hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Shetani, sambamba pamoja na wale wote wanaomfuata katika dhambi, watakavyoondolewa milele kutoka mbele za macho ya Bwana na watu wake, kufutiliwa mbali wasipate kuishi tena katika maangamivu ya mwisho ya kutisha ya dhambi na wadhambi kwenye ziwa la moto (angalia Malaki 4:1-3; Ufu 20:9-10, 13-15).

     Je, uko tayari jina lako na tabia kuja katika uchunguzi mbele ya Mungu katika wakati huu wa hukumu? Je, uko tayari Kristo amalize kazi yake ya upatanisho kwa ajili yako muda wowote? Je, uko tayari pamoja na dhambi zako zikiwa zimetubiwa, kusamehewa, na kufunikwa na damu ya Yesu Kristo kusudi uweze kuandaliwa kwa ajili ya ujio wake kuwapa ujira wake wa uzima wa milele wale wote ambao wamethibitisha wenyewe kuwa waaminifu mpaka mwisho (angalia Mathayo 10:22)?
     “Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye?” “Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.” “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake...” “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku za uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu…” “Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.” Malaki 3:2; Mithali 12:7; Warumi 5:1-2; Waefeso 6:13-18; Waebrania 4:7.