"LET THERE BE LIGHT" Ministries
home  |  Ugandan Tracts

UPENDO  WA  MUNGU  KWAKO  NA  KWANGU

     Vitu vya asili na ufunuo pamoja huthibitisha upendo wa Mungu. Baba yetu wa mbinguni ndiye chimbuko la uzima, la hekima, na la furaha. Hebu viangalie vitu vya ajabu na vizuri vya asili. Hebu fikiri jinsi vinavyokuwa tayari kubadilika kulingana na mahitaji na furaha. Mwanga wa jua na mvua, ambavyo hufurahisha na kunawirisha dunia, vilima na bahari na nyanda, vyote hunena kwetu juu ya upendo wa Mwumbaji. Ni Mungu ndiye hutoa mahitaji ya kila siku ya viumbe wake wote. Katika maneno mazuri ya mwimbaji wa zaburi:
     “Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kila kilicho hai matakwa yake.” Zaburi 145:15-16.

     Mungu alimfanya mwanadamu mtakatifu kamili na akiwa na furaha; na dunia ikiwa kamilifu, kama ilivyotoka katika mikono ya Mwumbaji; haikuwa na doa la uharibifu au kivuli cha laana. Ni uasi wa sheria ya Mungu--sheria ya upendo--ambao umeleta laana na mauti. Na bado hata katika maumivu yanatokanayo na dhambi, upendo wa Mungu hufunuliwa. Imeandikwa kwamba Mungu aliilaani ardhi kwa ajili ya mwanadamu (angalia Mwanzo 3:17). Mchongoma na miiba--mahangaiko na majaribu ambavyo hufanya maisha yake [mwanadamu] kuwa ya kuhangaika na kujishughulisha--vilipangwa kwa ajili ya kumsaidia kama sehemu ya mafunzo yanayohitajika katika mpango wa Mungu ili kumwinua kutoka katika uharibifu na kushushwa hadhi ambavyo vimeletwa na dhambi. Ulimwengu, pamoja na kuwa umeanguka, siyo wa huzuni na taabu. Katika [vitu vya] asili peke yake kuna ujumbe wa tumaini na furaha. Kuna maua juu ya michongoma, na miiba imefunikwa na [maua ya] waridi.
     “Mungu ni upendo” imeandikwa katika kila ua linalochanua, katika kila jani linalochipuka. Ndege wapendezao wanaofanya anga kuwa nzuri kwa nyimbo zao, maua yaliyoshenezwa kwa uzuri katika ukamilifu yakitoa harufu inukiayo hewani, misitu iliyosonga ya porini ambayo imeshehenezwa utajiri wa majani ya kijani--vyote vinathibitisha utunzaji wa karibu wa Baba; naam wa Mungu kuwafanya watoto wake wawe na furaha.
     Neno la Mungu hufunua tabia ya Mungu. Yeye mwenyewe ametangaza upendo wake usio na mfano na huruma. Wakati Musa alipoomba, “Nionyeshe utukufu wako,” Bwana alijibu, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako” Kutoka 33:18-19. Huu ni utukufu wake. Bwana alipita mbele ya Musa, na akatangaza, “BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi” Kutoka 34:6-7. Yeye si “mwepesi wa hasira, [bali] ni mwingi wa rehema,” “kwa maana yeye hufurahia rehema” Yona 4:2; Mika 7:18.


Mungu Ametuzunguka Sisi na Dalili za Upendo Wake

     Mungu amefunga mioyo yetu kwake kwa dalili zisizokuwa na hesabu mbinguni na duniani. Kupitia vitu vya asili, na mshikamano wa kina kikubwa na huruma ambao mioyo ya wanadamu inaweza kujua, ametafuta kujifunua mwenyewe kwetu. Na bado [vyote] hivi pasipo ukamilifu huwakilisha upendo wake. Hata kama vithibiti hivi vyote vimetolewa, adui wa mema hupofusha mawazo ya watu, kiasi kwamba humwangalia Mungu kwa woga; na kumfikiria [Yeye] kama mkali na asiyesamehe. Shetani huwaongoza wanadamu kumwona Mungu kama Mtu [Nafsi] ambaye furaha yake kuu ni kupatiliza haki,--mmoja mbaye ni hakimu [jaji] mkali, asiye na huruma, akipatiliza wenye makosa. Shetani anamchora Mwumbaji kama Nafsi Kuu inayochungulia kwa jicho la wivu ili kuona makosa na mapungufu ya wanadamu, ili kusudi aweze kushusha adhabu kwao. Ilikuwa ni kuondoa kivuli hiki cha giza, kwa kufunua kwa ulimwengu upendo usio na kipimo wa Mungu, ndipo Yesu alikuja kuishi kati ya wanadamu.
     Mwana wa Mungu alishuka kutoka mbinguni kumdhihirisha Baba. “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua” Yohana 1:18. “Wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia” Mathayo 11:27. Wakati mmoja wa mitume alipotoa ombi, “Utuonyeshe Baba,” Yesu alijibu; “Mimi nimekuwa pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Philipo?  Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yohana 14:8-9.
     Katika kueleza utume wake hapa duniani, Yesu alisema, Bwana “amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa” Luka 4:18. Hii ndiyo ilikuwa kazi yake. Alikwenda kila mahali akitenda mema na akiwaponya wote waliokuwa wamekandamizwa na Shetani. Hakukuwapo na vijiji vilivyo kamili ambavyo kulikuwa hakuna dalili za magonjwa katika nyumba yoyote, kwani alikuwa amepita kati yake na kuponya wagonjwa wao. Kazi yake ilitoa uthibitisho wa kupakwa kwake mafuta na Mungu. Upendo, rehema, na huruma vilifunuliwa katika kila tendo la maisha; moyo wake ulitoka katika kuwapa faraja wana wa wanadamu. Alichukua asili ya mwanadamu, ili aweze kukidhi mahitaji yetu. Maskini na wanyenyekevu hawakuogopa kumkaribia. Hata watoto wadogo walivutwa kwake. Walipenda kupanda juu ya magoti yake na kuangalia katika uso wake mwema, uliojazwa na huruma.
     Yesu hakupuuza neno hata moja la ukweli, lakini upendo ulikuwa mara zote katika moyo wake. Alitumia mbinu kuu zaidi na kufikiri, usikivu wa wema katika kuchangamana na watu. Hakuwa kamwe na hasira, hakusema kamwe bila uangalifu neno, wala hakutoa maumivu yasiyohitajika kwa roho iliyokuwa na usikivu. Alinena ukweli, na kwa wakati fulani akitoa makemeo ya kujenga kwa mioyo migumu kwa sababu aliwapenda sana kiasi kwamba hakuwa tayari kushusha chini ukweli au kubaki kimya. Alikemea unafiki, kutoamini, na uovu. Lakini bado aliulilia Yerusalemu, mji alioupenda, ambao ulikataa kumpokea, [Yeye aliye] Njia, Kweli, na Uzima. Walikuwa wamemkataa, Mwokozi wao, lakini aliwachukua katika wema wa huruma. Maisha yake yalikuwa ni yale ya kujinyima na kujali shughuli za wengine. Kila roho ilikuwa ya thamani machoni pake. Wakati alipojichukua mwenyewe kwa utu wa Ki-Mungu, alishuka kwa wema ili kuangalia kila mtu wa familia ya wanadamu. Katika watu wote aliona roho zilizoanguka ambazo ulikuwa ni utume wake kuziokoa.


Yesu--Ufunuo wa Upendo wa Mungu

     Hiyo ndiyo tabia ya Kristo kama ilivyofunuliwa katika maisha yake. Hii ndiyo tabia ya Mungu. Ni kutoka katika moyo wa Baba ambapo chemchemi za huruma ya Ki-Mungu, ikidhihirishwa katika Kristo, hububujika kwenda kwa wana wa wanadamu. Yesu, Mwokozi mwema, wa huruma, alikuwa Mungu “aliyedhihirishwa katika mwili” 1 Timotheo 3:16.
     Ilikuwa ni kwa ajili ya kutukomboa sisi ndipo Yesu aliishi na kuteseka na kufa. Alikuwa “mtu wa masikitiko,” ili tupate kufanywa washirika wa furaha yake ya milele. Mungu aliruhusu Mwana wake mpendwa, aliyejawa na neema na kweli, kuja kutoka katika ulimwengu wa utukufu usioelezeka, hadi katika ulimwengu ulioharibiwa na kuwekwa giza na dhambi, katika ulimwengu uliofanywa mweusi kwa kivuli cha mauti na laana. Alimruhusu kuacha kifua cha upendo wake, sifa za malaika, ili kuteseka kwa aibu, matukano, udhalilishaji, chuki, na mauti. “Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” Isaya 53:5. Mtazame akiwa jangwani, na pale Gethsemane, juu ya msalaba! Mwana wa Mungu asiye na doa alichukua juu yake mwenyewe mzigo wa dhambi. Yeye, aliyekuwa pamoja na Mungu, alihisi katika roho yake utisho wa kutengwa ambao dhambi hufanya baina ya Mungu na mwanadamu. Hii ilitoka katika midomo wakati wa kilio chake kikuu, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Mathayo 27:46. Ilikuwa ni mzigo wa dhambi, hisi za utisho wake mzito, za utengo wake wa roho kutoka kwa Mungu--ilikuwa ni [hali] hii ndiyo ilivunja moyo wa Mwana wa Mungu.

     Lakini kafara hii kuu haikufanywa ili kuumba katika moyo wa Baba upendo kwa mwanadamu, siyo kumfanya [Baba] awe tayari kuokoa. Hapana, hapana! “Maana Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” Yohana 3:16. Baba huonyesha upendo wake kwetu kwa kutoa kafara hii kuu ya Mwana wake kukuokoa wewe na mimi kutoka katika mauti ya milele. Kristo alikuwa ndiye daraja ambalo kupitia kwake Baba angemwaga upendo wake usio na kipimo kwa ulimwengu ulioanguka. “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake” 2 Wakorintho 5:19. Mungu aliteseka pamoja na Mwanawe. Katika kilio cha Gethsemane, kifo cha Kalvari, moyo wenye Upendo Usioelezeka ulilipa bei ya ukombozi wetu.
     Yesu alisema, “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena” Yohana 10:17. Hii inamaanisha, “Baba yangu amewapenda ninyi sana kiasi kwamba hata ananipenda Mimi zaidi kwa kuutoa uhai wangu ili kuwakomboa ninyi. Kwa kuwa Mbadala wako na Mkamilishaji, kwa kuusalimisha uhai wangu, kwa kuchukua udhaifu wako, maovu yako, nimethaminiwa na Baba; mtu wa hakika, kwani kutokana na kafara yangu, Mungu anaweza kuwa wa haki, na bado akawa Mthibitishaji wa yule anayemwamini.”


Ni Yesu Pekee Angeweza Kufunua Kikamilifu Upendo wa Mungu

     Hakuna yeyote isipokuwa Mwana wa Mungu tu ndiye angekamilisha ukombozi wetu; kwani ni yule tu aliyejua kimo na kina cha upendo wa Mungu ndiye angeudhihirisha. Hakuna chochote pungufu ya kafara isiyo na kifani iliyofanywa na Kristo badala ya mwanadamu aliyeanguka ndiyo ingeweza kueleza upendo wa Baba kwa mwanadamu aliyepotea.
     “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee.” Hakumtoa tu ili kuishi kati ya wanadamu, kubeba dhambi zao, na kufa dhabihu yao, lakini alimtoa kwa jamii iliyoanguka. Kristo angejishikamanisha na matakwa na mahitaji ya mwanadamu. Yeye aliyekuwa mmoja pamoja na Mungu amejishikamanisha mwenyewe na watoto wa wanadamu kwa kamba ambazo haziwezi kukatika kamwe. Yesu “haoni haya kuwaita ndugu zake” (angalia Waebrania 2:11). Yeye ni Kafara yetu, Mtetezi wetu, Kaka yetu, akibeba sura yetu ya kibinadamu mbele ya kiti cha enzi cha Baba, na katika zama za milele zote akiwa pamoja na jamii aliyoikomboa--Mwana wa Mtu. Na hii yote ni ili kwamba tuweze kuinuliwa kutoka katika uharibifu na kushushwa daraja na dhambi ili kusudi tupate kuakisi kwa wengine upendo wa Mungu na kushiriki furaha ya utakatifu.
     Bei iliyolipwa kwa ajili ya ukombozi wetu, kafara isiyo na mfano ya Baba yetu wa mbinguni kwa kumtoa Mwana wake kufa kwa ajili yetu, inapaswa itupatie sisi dhana za juu za vile ambavyo tunaweza kuwa kupitia kwa Kristo. Kama mtume Yohana aliyevuviwa alivyotazama kimo, kina, na upana wa upendo wa Baba kwa jamii inayoangamia, alijazwa na sifa na uchaji; na, akishindwa kupata lugha ya kueleza ukuu na huruma za upendo huu, aliita ulimwengu kuutazama [upendo huu]. “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu” 1 Yohana 3:1. Ni thamani ya namna gani hili linaweka juu ya mwanadamu!
     Kwa njia ya uasi tulikuwa mateka wa Shetani. Kwa njia ya imani katika dhabihu ya upatanisho ya Kristo tunaweza kuwa watoto wa Mungu. Kwa kuchukua asili ya mwanadamu, Kristo amemwinua mwanadamu. Wanadamu walioanguka wanawekwa mahali, ambapo kwa njia ya kushikamana pamoja na Kristo, wanaweza kweli kustahili jina “watoto wa Mungu.”
     Upendo kama huo hauna mfano wa kulinganisha. Watoto wa Mfalme wa mbinguni! Ahadi ya thamani! Dhamira ya juu sana kutafakari! Upendo usio na mfano wa Mungu kwa ulimwengu ambao haukumpenda Yeye! Fikra ina nguvu za kubadilisha juu ya roho na huleta mawazo kuwa mateka ya mapenzi ya Mungu. Kadiri tunavyojifunza zaidi tabia ya Mungu kwa mtizamo wa msalaba, ndivyo tunavyoona rehema zaidi, huruma, na msamaha uliochangamana na msamaha usiostahili na haki, na tunaona kwa wazi zaidi uthibitisho usioweza kuhesabika wa upendo ambao hauna mfano na huruma ukizidi ule wa mama mwenye huruma kwa mtoto wake aliyetanga mbali.
     Baba amedhihirisha waziwazi upendo wa milele kwako na kwangu (angalia Yeremia 31:3)! Je, hatutaruhusu mioyo yetu kuitikia upendo huu wa ajabu? Kwa kutoa mioyo yetu kwa Yesu tunaweza kuepuka kutoka katika uharibifu wa milele (2 Wathesalonike 1:8), na kwa kupitia Yeye kupata uzima wa milele (Yohana 4:14, 6:27, 12:50). Hatimaye tunaweza kuinua sauti zetu za milele katika sifa na shukrani kwa Mungu wa milele (Zaburi 106:48) na Mfalme wa milele (Zaburi 2:2, 6-7, 29:10; Yohana 1:49) pamoja na furaha ya milele (Isaya 35:10, 51:11) kadiri tunavyoingia ndani kupitia malango ya milele (Zaburi 24:7-10) katika ufalme wa milele (Zaburi 145:13; Danieli 4:3, 7:27; 2 Petro 1:11) kutembea milele pamoja na Mungu wetu na Mwokozi katika nuru ya milele ya mbinguni (Ufunuo 21:23-25; Isaya 60:19-20).